Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza kwa siku tatu mfululizo kesi ya Utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato chake, inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru,Godfrey Gugai.
Wakili kutoka (TAKUKURU) Vitalis Peter amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba,kuwa kesi hiyo ilitakiwa kuendelea lakini wameshindwa kuleta mashahidi kutokana na kutokuwa na taarifa kama Hakimu amemaliza likizo.
Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa ameiomba Mahakama itoe ahirisho fupi ili dhamira ya kumaliza kesi hiyo ionekane kwani wateja wake wamekaa ndani kwa muda mrefu.
Baada ya Maelezo hayo Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi tarehe itakayopangwa ili kesi hiyo ikamilike kwa wakati na washtakiwa waweze kujua hatma yao.Kesi hiyo imeairishwa hadi Februari 19,20 na 21, 2019.
Gugai na mwenzake watatu wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo, makosa 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.