Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ameagiza kukamatwa kwa, Kaissy Mkurugenzi wa Kampuni ya Seif for Tobacco Trading Co. Ltd aliyeingiza nchini makontena zaidi ya mia tano (500) yenye malighafi ya Molasesi iliyoharibika na kuyatelekeza katika Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Jafo ameagiza hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kushuhudia makontena hayo yakiwa yametelekezwa bandarini hapo na mengine kutawanywa katika baadhi ya bandari kavu jijini Dar es Salaam.
Amesema kamwe Tanzania haiwezi kugeuzwa kuwa dampo kwa kuruhusu bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo muda wake wa matumizi umeisha kuingizwa nchini kwa lengo la kutupwa kiholela.
“Ndugu zangu katika kusimamia mazingira hatuna mzaha, afya za binadamu na mimea ni dhamana yetu, sitaruhusu afya za watanzania kuwekwa rehani,” amesisiti Jafo.
“Kwa kuwa vipimo vilivyofanywa na TBS vinaonyesha kuwa Molasesi yote imekwisha haribika na ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira, namwagiza mfanyabiashara huyo kurudisha makontena hayo yalikotoka kwa gharama zake mwenyewe,” Jafo.