Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wiki tatu kwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuanza zoezi la upandaji wa miti kando ya barabara zilizopo Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Dkt. Jafo ametoa maelekezo hayo leo Desemba 31, 2021 alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo kwa ajili ya kukagua hali ya mazingira na kuipongeza TARURA kwa hatua iliyofikia katika ujenzi wa barabara hizo.
‘Hapa eneo la Serikali imewekeza takriban shilingi bilioni 89 kwa ajili ya kujenga miundombinu hii muhimu ya barabara sasa jukumu langu ni kuhakikisha eneo hili linakidhi matakwa ya kimazingira ikiwemo upandaji wa miti, sasa maelekezo yangu nataka mtumide mvua hizi zinazoanza kuneyesha muanze kupanda miti,” alisema.
Aidha, Waziri Jafo alisema kuwa barabara hizo zimejengwa kwa kiwango kinachotakiwa kwa kuwa na mifereji ambayo inasaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo unaoweza kutokea pindi mvua inaponyesha.
Alishauri ipandwe miti ya matunda ili kuweka mandhari nzuri ya Mji wa Serikali na kuwa haoni sababu ya kuchelewa kuanza kwa zoezi hilo hivyo aliagiza lianze mara moja.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Jamii wa TARURA, Dkt. Veronica Mirambo upo mpango wa upandaji mityi katika barabaa zote zilizojengwa katika eneo hilo.
Alisema baada shughuli iliyobaki ni kufukia ardhi iliyochimbwa wakati wa ujenzi pamoja na upandaji wa miti na majani ili kurejesha hali ya mazingira katika hali yake.
Pia Afisa Mazingira wa Jiji la Dodoma, Bw. Ali Mfinanga alisema Idara ya Mazingira kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati inaendelea na kampeni ya kuikijanisha Dodoma.
Aliongeza kuwa miongoni mwa maeneo inayoyafanyia kazi ni pamoja na barabara kadhaa na kuwa wanawashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za fedha kushiriki katika zoezi la upandaji miti