Michezo

Jamal Malinzi agoma kujiuzulu uenyekiti wake….

on

Jamal MalinziRAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema hatajiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA) pamoja na kuwa na majukumu ya kitaifa.

Katika taarifa yake aliyoitoa mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa KRFA mkoani hapa juzi Jumamosi, Malinzi alisema wakati anakuja kuhudhuria mkutano huo alikuwa na wazo la kujiuzulu.

Hata hivyo aliwaeleza wajumbe hao kuwa ameachana na wazo la kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa KRFA, kwa kuwa aliombwa na wajumbe asichukue hatua hiyo.

Alisema baadhi ya wajumbe wa KRFA walitishia kuachia nafasi zao endapo angejiuzulu nafasi yake ndani ya chama hicho ili aendelee kutumikia nafasi moja ya Rais wa TFF.

Pia alisema ameamua kuendelea ili kuzima uvumi kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka waliodai kuwa aligombea nafasi ya uenyekiti wa KRFA ili apate tiketi ya kugombea kiti cha urais wa TFF.

Katika hotuba yake kwa wajumbe hao Malinzi aliwataka kuhakikisha wanashirikiana na halmashauri za wilaya ili kutenga maeneo ya viwanja vya michezo na kusema Uwanja wa Kaitaba utawekewa nyasi bandia baada ya kupata ufadhili wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

SOURCE: MWANASPOTI

Tupia Comments