Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amempongeza Msajili wa Mahakama ya Rufani, Katarina Revocatus kwa kukataa kupokea kesi zenye mapungufu kisheria ikiwemo ile ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
Jaji Profesa Juma ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya sherehe za wiki ya Sheria na mwaka wa mahakama zinazotarajiwa kufanyika mjini Dodoma.
Jaji Profesa Juma amesema kuwa hawapendezwi na malalamiko ya jumla jumla yanayotolewa na watu hali ya kuwa kuna mfumo maalum wa mahakama wa kupokea malalamiko.
“Hauwezi kuwazuia Wanasiasa wasizungumze ndio kazi yao, sisi tunafanya kazi kimya kimya na ukitaka majibu utayakuta katika nyaraka,” amesema.
Pia amesema anamsifu Msajili huyo Katarina Revocatus kwa kusimama kidete na kukataa kusajili kesi zenye dosari, hivyo anampongeza kwa ujasiri.
Jaji Juma ametoa pongezi hiyo ikiwa ni siku chache tangu Msajili huyo alipokataa kupokea kesi ya Zitto Kabwe dhidi ya Spika wa Bunge kutokana na kuwa na dosari ikiwemo ya kutokuambatanishwa kwa kiapo cha Spika kwenda kwa Msajili.