Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema imepokea maombi ya leseni chini ya mfumo wa leseni kutaniko kutoka kwa Waombaji watatu wakiwemo Starlink Satellite Tanzania Limited kampuni inayomilikiwa na Tajiri namba moja Duniani ambaye ni Boss wa Makampuni ya SpaceX, Tesla na X (zamani Twitter), Elon Musk, ambaye ameomba leseni ya kitaifa ya miundombinu na leseni ya kitaifa ya huduma ya mifumo tumizi na kwenye taarifa hiyo Wanahisa wa kampuni hiyo wanatajwa kuwa ni Starlink Holdings Netherlands B.V na SpaceX Netherlands B.V.
Taarifa iliyotolewa leo November 15,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, imesema “Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta, Sura 306 ya sheria za Tanzania, maoni ya kimaandishi yanakaribishwa kutoka kwa yeyote kuhusiana na utoaji wa leseni kwa waombaji yafike TCRA ndani ya siku 14 tangu siku ya kutoka tangazo hili, maoni yatakayopokelewa yatazingatiwa na TCRA itakapokuwa inayafanyia kazi ombi hili”
Itakumbukwa February 24,2024 aliyekuwa Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye alisema Serikali ya Tanzania imeshatoa majibu kwa kampuni ya Starlink na vikao vinaendelea ili wakamilishe documents na waruhusiwe kuanza huduma zao Tanzania na kusema hakuna ukweli kwamba Starlink wanahujumiwa.