Watu wanne wamefariki na zaidi ya watu 200 kuhama makazi yao baada ya moto kuteketeza jengo la orofa tatu huko Jeppestown, mamlaka ya Afrika Kusini ilisema.
Tukio hilo lilitokea Jumapili asubuhi. Mamlaka inasema jengo hilo lilikuwa na watu wasio na vibali na kwamba watu watatu waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini.
Meya wa Johannesburg Dada Morero anasema hatua itachukuliwa kukabiliana na majengo yaliyotekwa nyara. “Jengo hilo ni jengo lililotelekezwa, kuna sehemu nyingi na mabati mengi ambayo wakazi wamekuwa wakiyatumia kugawanya jengo hilo.
“Hili eneo tulilopo ni la viwanda, kwa hiyo wanaligawanya kwa hizo partitions, kwa kutumia hizo karatasi kugawanya jengo zima, ili waweze kukaa. Kwa hivyo, jengo sio eneo la makazi, lakini ni jengo lililotelekezwa, ” Morero alisema.