Jeshi la Wanamaji la China limetoa onyo kwa Maafisa na Wanajeshi Vijana kuhusu hatari za kujiingiza katika mapenzi ya mtandaoni na kucheza kamari ya Mtandaoni ambapo onyo hili liliwalenga hasa wale waliozaliwa baada ya 1990, na linawahimiza kutoonyesha utambulisho wao wa kijeshi Mtandaoni kwa sababu wanaweza kuwa rahisi kudanganywa na Wahalifu.
Jeshi limeeleza kuwa maadili ya kijeshi yanahitaji usiri, hivyo wanajeshi wanapaswa kuepuka kujihusisha na urafiki mtandaoni na Watu wasioaminika na Onyo lingine ni kuhusu kamari ya Mtandaoni, ambayo ni kinyume cha sheria Nchini China, ambapo uraibu wa kamari umeelezwa kuwa unaweza kuleta madeni yasiyokwisha.
Kwa upande mwingine, Rais Xi Jinping amekuwa akionya kuhusu matatizo ndani ya jeshi, ikiwa ni pamoja na ufisadi na ukosefu wa nidhamu pia alisisitiza umuhimu wa uaminifu kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) kutoka kwa maafisa waandamizi wa kijeshi.
Hatimaye, Rais Xi amewataka maafisa waandamizi kufanya tathmini ya ndani, kutafakari kwa kina na kufanya marekebisho ya kweli ili kuondoa matatizo yaliyopo ndani ya Jeshi.