Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limetangaza mafanikio makubwa dhidi ya kundi la Waasi wa M23 katika Mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki, Jeshi la Congo limefanikiwa kuwafurusha Waasi hao kutoka maeneo muhimu ambayo walikuwa wameyadhibiti.
Msemaji wa Jeshi la Congo, Guillaume Ndjike Kaiko amethibitisha maendeleo haya akisema kuwa maeneo kadhaa yaliyokuwa chini ya udhibiti wa M23 sasa yamewekwa chini ya Mamlaka ya Serikali huku akisisitiza kuwa Jeshi linaendelea kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano lakini litachukua hatua kila mara linaposhambuliwa na Vikosi vya M23 au Wanajeshi wa Rwanda.
Waasi wa M23, ambao walijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na hata kufanikiwa kuliteka jiji la Goma kwa muda mfupi, jina la Kundi hilo linatokana na makubaliano ya amani ya Machi 2009 ambayo M23 inadai Serikali ya Congo haikuyatekeleza na baada ya kipindi cha utulivu, M23 ilirejea tena mwishoni mwa mwaka 2021 ikiteka maeneo makubwa mashariki mwa Congo.
Umoja wa Mataifa umewahi kuishutumu Rwanda kwa kuwasaidia Waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekana mara kwa mara ambaye pia Rais wa Rwanda, Paul Kagame hivi karibuni alitoa wito wa mazungumzo kati ya Serikali ya Congo na Waasi wa M23 ili kupata suluhisho la amani kwa mgogoro huo.
Wakati mapigano yakiendelea, Jumuiya ya kimataifa inaendelea kuwa na wasiwasi kuhusu athari za Kibinadamu hasa kwa mamia ya maelfu ya Watu waliolazimika kuyahama makazi yao pia Serikali ya Congo imeapa kuendelea kulinda uhuru wa Taifa hilo na kuwahakikishia usalama Raia wake dhidi ya vitisho vya ndani na nje.