Viongozi wa Afrika Mashariki wamekubaliana jana Jumatatu kutuma jeshi la kikanda la Afrika Mashariki kwenda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kutoa wito wa mapigano kusitishwa mara moja.
Hatua hiyo ilitangazwa na ofisi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta baada ya Wakuu wa Mataifa saba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya mazungumzo mjini Nairobi kuhusiana na kuongezeka kwa machafuko mashariki mwa Congo.
Kulingana na ofisi hiyo ya Rais Uhuru Kenyatta, Wakuu hao wameliagiza Jeshi hilo la kikanda kushirikiana na vikosi vya Congo kurejesha utulivu na kuhakikisha amani inapatikana.
Hata hivyo taarifa hiyo haikusema iwapo Rwanda inayolaumiwa kuwasaidia Waasi itaunganishwa kwenye Jeshi hilo, ingawa Serikali ya Congo inasisitiza haitakubali Wanajeshi wa Rwanda kujumuishwa.