Takriban Wapalestina watatu waliuawa wakati jeshi la Israel liliposhambulia kwa bomu shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao katikati mwa Gaza mapema Jumapili.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Wafa, jeshi la Israel lililenga orofa ya juu ya Shule ya Khalid bin al-Walid huko Nuseirat.
Shambulio hilo pia liliacha wengine wengi kujeruhiwa.
Siku moja kabla, jeshi la Israel lilishambulia kwa mabomu shule nyingine inayohifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao, Shule ya Kefr Kasim katika kambi ya wakimbizi ya al-Shati magharibi mwa Gaza City, na kuua Wapalestina sita.
Jeshi la Israel mara nyingi hulenga shule zinazohifadhi watu waliokimbia makazi yao katika Ukanda wa Gaza.
Tangu Oktoba 7 mwaka jana, mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yamegharimu maisha ya Wapalestina 41,431, wakiwemo watoto 16,795 na wanawake 11,378, huku watu 95,818 wakijeruhiwa.
Maelfu bado wanasadikiwa kukwama chini ya vifusi huku hospitali na taasisi za elimu ambako raia wametafuta makazi zikiendelea kulengwa, na kuharibu vibaya miundombinu ya eneo hilo.