Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ubia wa Elimu Duniani (GPE) ameshiriki Mkutano wa Mwaka 2024 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB 2024 Annual Meeting) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya tarehe 26 – 28 Mei, 2024. Ametumia fursa ya kushiriki Mkutano huo kuzungumza na vongozi mbalimbali, hususan kutoka sekta za kifedha, sekta binafsi na washirika wa kimaendeleo kuhusu umuhimu wa kuongeza ufadhili wa kifedha ili kuimarisha mpango wa utoaji chakula kwa wanafunzi wakiwa mashuleni pamoja na kuhamasisha ubunifu wa mbinu mpya za kufadhili elimu ya juu, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Taasisi ya GPE ambayo Rais Mstaafu Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi imejikita katika kujenga ubia na wadau mbalimbali wa kimataifa na ndiyo Taasisi kinara duniani inayohamasisha jitihada za kuzisaidia nchi zaidi ya 76 kuimarisha mifumo yao ya elimu ili kutoa elimu bora zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume, hususan wale wanaotoka katika mazingira duni, wenye ulemavu na wanaoathiriwa na majanga kama vile vita na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wa Afrika, GPE ina miradi inayozunufaisha nchi 40, ikiwemo Tanzania. Tangu mwaka 2016 hadi sasa, Taasisi ya GPE imetoa msaada wa zaidi ya shilingi bilioni 250 za Kitanzania kufadhili programu hiyo ya utoaji wa chakula mashuleni katika nchi inapofanya shuhuli zake.
Katika Mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Rais Mstaafu Kikwete alieleza umuhimu wa washiriki kufikiria mbinu mpya za kupata fedha zitakazotumika kugharamia programu za kutoa chakula mashuleni kwani ukweli ni kwamba licha ya jitihada kubwa inayofanyika na nchi nyingi za kipato cha chini na kati katika kuimarisha programu hiyo, bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kuelemewa na madeni.
Akaeleza kuwa programu ambayo ni moja ya mikakati muhimu ya kielimu inayoongeza mahudhurio ya watoto mashuleni na kukuza uelewa wa wanafunzi inasaidia pia katika kukabiliana na tatizo la udumavu na unyafuzi linalolikabili bara la Afrika. Aidha, aliwakumbusha washiriki kuwa msingi wa bara la Afrika na Dunia kufikia malengo waliyojiwekea kama vile lengo la Umoja wa Afrika la Ajenda 2063 (Afrika Tunayoitaka) na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ni kuwekeza katika elimu ili kuwaandaa watoto na kuwajengea uwezo wa kupambana, kuishi na kustawi katika mazingira mapya ya karne ya 21.
Mkutano huo unaofanyika kila mwaka ulihudhuriwa na Mawaziri wa Fedha na wa Elimu kutoka nchi mbalimbali duniani, viongozi kutoka Umoja wa Afrika na Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika, wawakilishi wa mashirika ya kimaendeleo kama vile Rockefeller Foundation, Shirika la Chakula Duniani (WFP), Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) pamoja na viongozi wa sekta binafsi kutoka barani Afrika.