Mapato ya uuzwaji vitalu vya uwindaji yameongezeka na kufikia Dola za Kimarekani milioni 8.32 kutoka milioni 2.26 sawa asilimia 267.1 baada ya Serikali kutumia njia ya mnada.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 23, 2022 katika Chuo Cha Utalii Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema mapato hayo ni kutoka katika minada sita iliyofanyika kuanzia 2019 na kuongeza kuwa mdana mwingine utafanyika kuanzia Machi 2022.
Amefafanua kuwa katika mnada huo ulijumuisha vitalu 75 vya uwindaji wa kitalii, ambapo vitalu 49 umiliki wake unamalizika Desemba mwaka huu, na 26 ni vitalu vilivyokuwa wazi.
Amesema kampuni 26 kati ya 39 zilizoshiriki mnada huo zilishinda vitalu vya uwindaji 45. Amesema katika mnada huo Dola milioni 6.199 zilikusanywa, kati ya fedha hizo Dola 170,000 zilikusanywa kutokana na ada za maombi ya ushiriki na Dola milioni sita zimetokana na ada ya vitalu.
Aidha, ameongeza kuwa ugawaji wa vitalu kwa njia yam mnada umewezesha upatikanaji wa soko na thamani halisi ya rasilimali muhimu ya taifa ya vitalu vya uwindaji kitalii.
Mary Masanja amesema kuwa hatua hiyo imekuja kutokana na baadhi ya watu kulalamikia njia ya kiutawala kugawa vitalu hivyo na hivyo mwaka 2018 Serikali ilifanya tathmini nakuona njia bora ya kugawa vitalu ni njia yam nada.