José Mourinho yuko tayari kuchukua mikoba ya Bayern Munich ikiwa Thomas Tuchel atafukuzwa.
Bayern ni ya pili katika Bundesliga, baada ya kuchapwa 3-0 na viongozi Bayern Leverkusen wikendi hii, jambo ambalo lilizidisha shinikizo kwa Tuchel. Klabu hiyo sasa iko nyuma kwa pointi tano.
Mourinho, 61, aliondoka Roma katika klabu ya Serie A mwezi uliopita, huku nguli wa klabu hiyo Daniele De Rossi akiteuliwa kama mbadala wake wa muda hadi mwisho wa msimu.
Mkataba wa Mourinho ulimalizika mwishoni mwa msimu huu lakini, kufuatia kushindwa kwao 3-1 na AC Milan, na klabu hiyo ikiwa katika nafasi ya tisa kwenye Serie A, wamiliki na meneja waliachana. Ilihitimisha maisha ya Mourinho katika klabu hiyo, iliyoanza Mei 2021 na kumfanya kushinda taji la Ligi ya Europa Conference mnamo 2022 na kufika fainali ya Ligi ya Europa msimu uliopita.
Mourinho alijiunga na Roma mwaka 2021 kufuatia kazi yake aliyoifundisha FC Porto, Chelsea (mara mbili), Inter Milan, Real Madrid, Manchester United na Tottenham. Alichukua kazi ya Roma siku 15 tu baada ya kutimuliwa Spurs.