Idadi ya waliofariki katika ibada ya kila mwaka ya Hija, ambayo ilifanywa katika joto kali nchini Saudi Arabia, imeongezeka na kufikia 900.
Mwanadiplomasia wa Kiarabu aliliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatano kwamba vifo miongoni mwa Wamisri pekee vimepanda hadi “angalau 600” kutoka zaidi ya 300 kwa siku iliyotangulia, hasa kutokana na joto kali.
Idadi hiyo ilileta jumla ya walioripotiwa kufariki kufikia 922, kulingana na takwimu za AFP zilizotolewa na nchi mbalimbali.
Mwanadiplomasia huyo baadaye aliongeza kuwa maafisa wa Misri nchini Saudi Arabia wamepokea “ripoti 1,400 za mahujaji waliopotea”, wakiwemo 600 waliofariki.
Mabrouka bint Salem Shushana wa Tunisia, akiwa na umri wa miaka 70, ametoweka tangu kilele cha ibada ya Hija Jumamosi katika Mlima Arafat, mumewe Mohammed aliambia AFP siku ya Jumatano.
Kwa sababu hakuwa amesajiliwa na hakuwa na kibali rasmi cha Hijja, hakuweza kufikia vituo vya kiyoyozi vinavyoruhusu mahujaji kupoa, alisema.
Facebook na mitandao mingine ya kijamii imefurika picha za waliopotea na kuomba taarifa zao.
Hija ni moja ya nguzo tano za Uislamu na Waislamu wote wenye nyenzo lazima waikamilishe angalau mara moja.