Mix

Rais Magufuli ataka Watanzania waliofungwa nje kwa dawa za kulevya waachwe

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha vinasimamia sheria ipasavyo ili kukabiliana na tatizo hilo hapa Tanzania.

Ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Rogers William Siyanga, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Joseph Edward Sokoine, Balozi wa Tanzania Algeria Mhe. Omar Yusuf Mzee na Balozi wa Tanzania Uganda Grace Aaron Mgovano.

Pia Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wa Serikali kuungana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na ametaka mapambano hayo yasifanywe kwa mzaha wala kwa kuangalia majina ya watu, vyeo vyao na taasisi wanazoongoza.

Vilevile Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na amewaomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya biashara na kutumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya Taifa.

“Niwaombe ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya, waandishi wa habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania wetu, akitokea mtu anapambana na dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya kumchafua”

“Vita hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na Serikali itahakikisha inasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Anna Makinda na sheria hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria hii.”

Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha kuna watanzania 1,007 wamekamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, na amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kutojihusisha kuwatetea waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake waache sheria za nchi husika zichukue mkondo wake.

VIDEO: Paul Makonda ataja mbinu zinazotumiwa kuingiza dawa za kulevya Tanzania, bonyeza play kwenye hii video hapa chini kufahamu

BREAKING NEWS zote na stori za mastaa utazipata kwa Reporter wako Millard Ayo, hakikisha umejiunga na mimi kwenye Facebook, Twitter, Instagram, Snapchat, Youtube, APP kwenye ANDROID na IOS kote huko kwa jina hilohilo la @millardayo

Soma na hizi

Tupia Comments