Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni leo amewasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni kwamba katika kipindi cha mwezi July, 2022 hadi May, 2023 makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika Vituo vya Polisi yameongezeka.
“Pamoja na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu nchini, uhalifu wa makosa dhidi ya binadamu, maadili ya jamii na kuwania mali umeendelea kuwepo, katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika Vituo vya Polisi yalikuwa 45,455 ikilinganishwa na makosa 43,771 yaliyotolewa taarifa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22”
“Hili ni ongezeko la makosa 1,684 sawa na 3.8%, ongezeko la makosa haya makubwa linatokana na Watu kujichukulia sheria mkononi, wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, migogoro ya ardhi na mirathi, mmomonyoko wa maadili na tamaa ya mapenzi, hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kuzingatia sheria, kuhamasisha jamii kutoa taarifa za makosa hayo kwa wakati kwa kushirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na kushirikisha Viongozi wa Dini katika kutoa elimu ya maadili mema kwa Jamii”
“Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023, jumla ya mashauri ya Jinai 45,455 yameshughulikiwa, mashauri 19,671 yalifikishwa Mahakamani, ambapo 4,400 yameshinda, 545 yalishindwa, mashauri 41 yaliondolewa Mahakamani na 14,685 yanaendelea kusikilizwa Mahakamani”