Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Wananchi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imefanya oparesheni maalum Mkoani Morogoro kwa muda wa siku tisa katika vijiji vya Nyarutanga, Lujenge na Mafumbo vilivyopo Wilaya za Morogoro vijijini na Kilosa ambapo katika vijiji vya Mafumbo na Lujenge Mamlaka imeteketeza jumla ya ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi.
Katika oparesheni iliyofanyika kijiji cha Nyarutanga Watu 6 wakiwa na kilogramu 342 za bangi wamekamatwa na watafikishwa Mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Akiongea baada ya uteketezaji wa mashamba hayo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa pembezoni mwa Mto Mbakana, Misigiri na Mgeta kwenye eneo la akiba la Hifadhi ya Taifa Mikumi.
“Uharibifu mkubwa sana wa mazingira umefanyika katika eneo hili ambapo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi na hivyo kuharibu uoto wa asili, pia uharibifu uliofanyika katika eneo la akiba la Mikumi unaharibu ikolojia ya eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa uoto wa asili na ikizingatiwa Mito hiyo inatiririsha maji katika Bwawa la Mwakimu Nyerere linalotegemewa kwa uzalishaji wa umeme”
Lyimo amewashukuru sana Wananchi hususan Vijana waliojitolea kushiriki katika zoezi zima la uteketezaji wa mashamba ya bangi pamoja na Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka kuweza kufanya operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi na kutokomeza dawa za kulevya Tanzania.