Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema jumla miti milioni 686.24 iliyopandwa katika halmashauri mbalimbali nchini imestawi.
Amesema kuwa miti iliyopandwa na kustawi ni sawa na asilimia 82.3 ya miti yote milioni 866.7 iliyopandwa katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 023/2024.
Mhe.Khamis amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Februari 05, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Tunza Malapo ambaye alitaka kujua kama Serikali imefanya tathmini ya kujua ni miti mingapi inayopandwa inatunzwa na kukua ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, imekuwa ikifanya tathmini ya upandaji miti kwa kila mwaka ili kukabiliana na uharibifu wa ardhi, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kuwa katika msimu wa mwaka 2024/25 Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kubaini idadi ya miti iliyopandwa na iliyostawi kwa maeneo yote nchini.
Aidha, Mhe. Khamis amedokeza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi na sekta binafsi kuendelea kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutunza mazingira.
Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa jamii nzima ya Watanzania kutumia mvua zinazonyesha kipindi hiki kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.