Juventus wataweza kusitisha mkataba wa Paul Pogba na klabu hiyo iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United amesimamishwa kwa muda na klabu hiyo ya Italia baada ya kufeli majaribio ya kuzuia matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku mwezi uliopita.
Pogba alirejesha mtihani ambao ulikuwa na viwango vya juu vya testosterone wakati wababe hao wa Italia walipocheza na Udinese mnamo Agosti 20.
Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli, anaweza kupigwa marufuku kati ya miaka miwili na minne.
Na ripoti kutoka Gazzetta dello Sport inadai Juve watakuwa na uwezo wa ‘kufuta kandarasi yake’ ikiwa hilo litatokea.
Pogba alirejea Juventus majira ya kiangazi mwaka jana, akisaini mkataba wa miaka minne hadi 2026, lakini uhamisho huo haujafanikiwa kutokana na kiungo huyo kucheza mechi 11 tu tangu wakati huo, bila bao wala pasi za mabao.
Iwapo Pogba atathibitika kuwa na hatia na kandarasi yake ya Juventus kubatilishwa, itamaanisha kuokoa euro milioni 30 kwa wababe hao wa Serie A.