Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo December 05 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani Jim Deboo ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo.
Baada ya Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao.
“Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao”;- Rais Magufuli.
Rais Magufuli ametaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itazinunua kuwa ni ndege 1 aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni, 2018. Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.
Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.
“Tumeleta ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi 200,000/- wakati nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo”- Rais Magufuli.
AyoTVMAGAZETI: Rais atoa neno zito kwa mahasimu wa JK, Lowasa atia ubani uamuzi wa JPM, Bonyeza play kuungana na Alice Tupa kwenye video hii hapa chini