Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kujisomea vitabu kwa ajili ya kujiongezea maarifa mbalimbali ikiwemo mbinu za kujiendeleza kiuchumi.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho ‘I Am Positioned’ kilichoandikwa na mwandishi Leah Karunde, ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kodi, Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) David Kafulila amesema taifa linaweza kuendelea kwa kuwa na watu wenye maarifa, licha ya kuwepo kwa rasilimali za kutosha.
“Kitabu hiki kina mambo mengi mazuri sana ikiwemo kuhusu uhuru wa kifedha, uwekezaji na nidhamu ya matumizi,”
“Hivyo ni vema watu wakakisoma kwa sababu kina mambo mengi ya kujifunza katika kujiendeleza kiuchumi,”
“Tunahitaji kuwa na jamii yenye mtazamo chanya kuhusu masuala ya kifedha ili kuwa na nidhamu katika matumizi yake kwa kuwekeza maeneo mbalimbali,” amesema Kafulila.
Ameongeza kuwa kuna fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowekwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, akiwataka wananchi kuzichangamkia na kuongeza kuwa kitabu hicho ni sehemu ya mwongozo katika kuisadia jamii kufikia malengo ya kibiashara, nidhamu ya fedha na uwekezaji.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasomi mbalimbali wakiwemo washauri wabobevu katika masuala ya kifedha, Bi Leah amesema kuwa kitabu hiki pamoja na mambo mengine, kinawajengea uwezo wa kifedha watu mbalimbali wakiwemo vijana katika kukuza uchumi katika ngazi binafsi, familia na jamii kwa ujumla.
“Kitabu hiki hakifundishi kuhusu pesa tu, bali pia kinafundisha namna ya kujiwekea malengo, ustahimilivu, maarifa yanayoweza kutumika katika kujenga misingi imara ya kifedha, kuunda vyanzo vingi vya mapato, na kujifunza mbinu za kuokoa pesa na kuwekeza.
”Lakini pia kina hadithi binafsi zinazoelezea namna ya kushinda changamoto mbalimbali na zinazoelezea changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana barani Afrika na kutoa ramani ya mabadiliko ya biashara za familia kuwa mashirika yanayostawi.
”Lengo langu ni kuwasaidia watu wengine , kupitia kitabu hiki na kuhamasisha jamii kufikia mafanikio ya kifedha katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia ya kuboresha maisha kwa Watanzania,” amesema Bi Leah.