Waziri wa Nishati, January Makamba mapema leo amekutana na kufanya kikao na Bi. Nina Koch akiwa Dodoma ili kuzungumzia maandalizi ya Uwekezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG).
Waziri Makamba amesema anaridhishwa na hatua iliyofikiwa na kusisitiza kuwa anatarajia kuona mradi huu ukitekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa ambapo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa Bi. Koch amesisitiza kuwa Equinor ipo tayari kutoa ushirikiano katika uanzishaji wa Ofisi Maalum ya Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi asilia (LNG Project Office) ambayo itasimamia na kuratibu shughuli za mradi katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji.
Bi. Kochi amesema >> “kwa uzoefu wangu miradi kama hii, sio rahisi kukubalika moja kwa moja na pande zote yaani Kampuni na Uongozi wa Nchi. Lakini kwa mradi huu, uongozi wa kisiasa na wananchi wote wa Norway wanauunga mkono’ – Bi. Koch.
Kwa sasa timu za majadiliano za upande wa Serikali ya Tanzania na wawekezaji zipo katika hatua ya Uandishi (drafting) ya mikataba ya mwisho (final agreements)
Katika ziara yake nchini, Bi. Koch alitembelea eneo utakapojengwa mradi huo wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG) mkoani Lindi.
Bi Koch aliipongeza Serikali kwa kuchagua eneo la mradi karibu na kiwanja cha ndege, jambo ambalo litarahisisha usafiri wa wafanyakazi na vifaa mbalimbali wakati wa ujenzi na uendeshaji wa mradi.
Pia Bi. Koch alitembelea Chuo cha VETA Lindi ambapo Kampuni zinazotarajiwa kuwekeza katika mradi wa LNG, zimekuwa zikitoa ufadhili wa vifaa vya kujifunzia.
Alimueleza Waziri Makamba kuwa lengo la Kampuni ya Equinor ni kuendelea na kuvifadhili vyuo mbalimbali hasa vya mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuwajengea uwezo kwa Watanzania waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi na uendeshaji wa mradi wa huo wenye thamani ya zaidi ya trilioni 70.
Katika kikao hicho Waziri Makamba aliambatana na Kamishna wa Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati, Bw. Mike Mjinja pamoja na Mha. Charles Sangweni Mkurugenzi Mkuu wa PURA. Kwa upande wa Equinor, Bi Koch aliongozana na Bw. Nizar Damree, Mkuu wa Kitengo cha Mkondo wa Juu Kimataifa,Bw. Nizar Damree Mkuu wa Kitengo cha mkondo wa juu kimataifa, Bi. Unni Fjær Makamu wa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Equnor Tanzania pamoja na Bi. Genevieve Kasanga, Afisa Mawasiliano Equinor Tanzania.