Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo leo wameitembelea Kampuni ya Sukari Kilombero mkoani Morogoro ili kujionea maendeleo ya mradi wa kimkakati ya upanuzi wa kiwanda cha K4.
Lengo la ziara hiyo likiwa ni kushuhudia uwekezaji huu wa kimkakati katika kiwanda hiki kikubwa cha sukari, ambacho kinalenga kusaidia dira ya Tanzania ya kujitosheleza kwa uzalishaji wa sukari ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji na matumizi ya sukari na kuongeza fursa za masoko kwa wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero.
Ziara hii muhimu ni sehemu ya juhudi za serikali ya Tanzania na Bunge katika kuhimiza uwekezaji wa kimkakati na kuhakikisha kwamba mazingira ya uwekezaji, sera, na utawala ni rafiki katika kusaidia utekelezaji wa miradi hii kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
Mradi wa upanuzi wa kiwanda cha K4, wenye thamani ya TZS bilioni 732, unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 127,000 hadi tani 271,000, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa sukari nchini.
Aidha, uhitaji wa miwa kutoka kwa wakulima wa Kilombero utaongezeka kutoka tani 600,000 hadi tani 1,500,000. Mradi huu pia utaimarisha uzalishaji wa nishati, ambapo hadi MW 10 za umeme zitaunganishwa kwenye gridi ya Taifa, huku msimu wa uzalishaji ukipunguzwa kutoka wiki 42 hadi wiki 32 ili kuendana na vipindi vya mvua.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mheshimiwa Deodatus Mwanyika (MB), ameipongeza Kampuni ya Sukari Kilombero kwa mchango wake katika kuimarisha sekta za viwanda na kilimo, amesema:
“Huu ni mfano bora wa uwekezaji wenye tija ambao utachochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya wakulima wa miwa, huku pia ukishughulikia upungufu wa sukari nchini. Hongereni wawekezaji na uongozi mzima wa Kilombero kwa hatua hii kubwa.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Sukari Kilombero, Balozi Ami Ramadhan Mpungwe, ametoa shukrani kwa ziara hiyo, akisema:
“Tunajivunia kuwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge, uongozi wa mkoa wa Morogoro, na wawakilishi wa wilaya ya Kilombero. Ziara yenu ina maana kubwa kwetu na kwa uwekezaji huu wa kimkakati. Huu ni uwekezaji wa kihistoria katika sekta ya sukari na wa kipekee katika Afrika ya Mashariki na kati, ambapo mwekezaji amewekeza zaidi ya dola milioni 306 katika mradi mmoja. Hii inathibitisha dhamira yetu kama kampuni katika kusaidia azma ya taifa ya kujitosheleza kwa sukari ifikapo 2025.”
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero, Guy Williams, wakati wa kikao cha kutoa taarifa za kibiashara, ameeleza kuwa mradi huu unatarajiwa kuanza katikati ya mwaka huu, huku maendeleo yake yakiwa yamefikia asilimia 95.
Williams amebainisha kuwa mradi huu utaongeza ajira katika mnyororo wa thamani, ambapo asilimia 60 ya miwa inayosagwa katika kiwanda cha K4 itatoka kwa wakulima wa bonde la Kilombero, huku asilimia 40 ikitoka kwenye mashamba ya kampuni.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima, ameusifu uwekezaji huu wa kimkakati katika sekta ya sukari mkoani Morogoro, akisisitiza kuwa mkoa huo una mchango mkubwa katika uzalishaji wa sukari nchini.
Amesema kuwa serikali ina jukumu la kuendelea kuimarisha na kulinda uwekezaji kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kampuni ya Sukari Kilombero itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali na wadau wengine kuhakikisha mradi wa upanuzi wa K4 unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa ya muda mrefu kwa taifa.