Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar, imelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa utendaji kazi madhubuti katika usimamizi wa sheria na kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira wa usafiri majini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahya Rashid Abdulla, leo tarehe 03 Februari 2025, walipotembelea Ofisi za TASAC mkoani Tanga na kufanya kikao na watumishi wa TASAC pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
“Tumefurahishwa na utendaji kazi mzuri wa TASAC katika udhibiti na usimamizi wa safari kwa njia ya maji hasa katika Bandari hii ya Tanga ambayo kwa kiasi kikubwa imerahisisha usafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani kwa eneo hili la mwambao ambalo lilikua na changamoto kubwa ya usafiri kwa njia ya maji,” amesema Mhe. Abdulla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, Meneja Mafunzo na Utoaji vyeti Mha. Lameck Sondo ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendeleza weledi, ufanisi na mashirikiano katika kudhibiti shughuli za usafiri majini kwa maslahi mapana ya Taifa.