Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Augustine Vuma Holle (Mb) amesema Kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya utalii inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA katika Hifadhi ya eneo la Makuyuni Wildlife Park iliyopo wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.
Mhe. Augustine ameyasema hayo leo Februari 9, 2025 wakati Kamati yake ilipotembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAWA katika eneo hilo.
“Kamati imefurahishwa na namna ambavyo miradi inaendelea, ikumbukwe kwamba hili eneo mara ya kwanza lilikuwa chini ya mwekezaji Kwa muda mrefu sana, baada ya Serikali kuona kwamba hakuna tija eneo hili kuendelea kukaa Kwa mwekezaji, ikalichukua eneo hili na kukabidhiwa msajili wa hazina lakini baadae msajili wa hazina aliwakabidhi TAWA ili waweze kuliendeleza” amesema Mhe. Augustine
“Kamati imeona na imeshuhudia pasipo na shaka kwamba uwekezaji unafanyika na unafanyika kwa utaratibu ambao unafaa na kwakweli tija ya uwekezaji ipo kwasababu mapato yameanza kuongezeka na tunaamini yataendelea kuongezeka. Kwahiyo TAWA wataendelea kufanya uwekezaji hapa kwasababu tumeona kwamba imeanza kulipa” ameongeza
Aidha Mwenyekiti huyo wa Kamati ya PIC ametoa wito Kwa watanzania wote na wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani na Arusha kutembelea eneo hilo ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.