Februari 27, 2023, Dar es salaam, Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika hapa nchini (TCDC) imeanza kutekeleza mpango ya kubadili namna ya kuendesha vyama vya ushirika na kuviwezesha kutumia teknolojia za kisasa katika kufanya shughuli zao
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika hapa nchini Abdulmajid Nsekela ametoa taarifa hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa ushirika kujadili maendeleo ya ushirika na kuweka mkakati wa kuimarisha sekta ya hiyo hapa nchini
Nsekela amesema uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya kidijitali itaongeza ufanisi wa kiutendaji katika Vyama vya Ushirika, pamoja na Mamlaka za Usimamizi wa sekta hiyo.
Ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine lakini mapendekezo yatakayotolewa katika mkutano huo yatasaidia kuuboresha mfumo wa ushirika kuwa wa kisasa zaidi na ili kuwawezesha wananchi kushiriki ipasavyo kwa ustawi wao na wa Taifa kwa ujumla.
“Ni matumaini yangu kuwa Maazimio yatakayofikiwa kupitia Mkutano huu yatapaswa kutekelezwa ipasavyo na kila mdau na kwamba taarifa ya utekelezaji itakuwa inatolewa na kujadiliwa mara kwa mara”-amesema Nsekela.
Kwa upande wake Mrajisi wa Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege amesema lengo kubwa la mkutano huo wa wadau wa ushirika ni kujadili maendeleo ya ushirika na kuweka mkakati wa kuimarisha sekta hiyo hapa nchini.
“Mkutano huu ni muhimu kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Ushirika hapa nchini, lakini pia tumekutana wadau wote ili kuja na mapendekezo ya pamoja ya kuendeleza sekta hii kwa maendeleo ya Taifa”- amesema Ndiege