Kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing ya nchini Marekani imekabidhi ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F kwa Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania (TGFA) tayari kwa safari ya ndege hiyo kutoka Marekani na kuja hapa nchini Tanzania.
Makabidhiano hayo yamefanywa katika kiwanda Boeing kilichopo Jiji Seattle nchini Marekani kwa Wawakilishi wa Serikali ya Tanzania ambao ni Balozi wa Tanzania Washington, Marekani Mhe. Elsie Sia Kanza, Mtendaji Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TGFA Capt. William Budodi.
Ndege hiyo ya mizigo aina ya Boeing 767-300F ndio ndege ya kwanza kununuliwa hapa Barani Afrika, na ni ndege iliyojibebea sifa lukuki katika usafirishaji wa mizigo kwa kutumia anga Duniani.
Boeing 767 -300F ina uwezo wa kubeba tani 54 za mizigo na kuruka kwa masaa 10 ambapo ndege hiyo inatarajiwa kuwasili nchini mnao tarehe tatu Juni huku mapokezi ya ndege hiyo yanatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Ndege hiyo imenunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya matumizi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)