Baraza la Maaskofu wa Katoliki Kenya (KCCB) limekataa mchango wa Shilingi za Kenya milioni 5.6 (takriban Shilingi za Kitanzania milioni 104) uliotolewa na Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, wakati wa ibada katika Kanisa Katoliki la Soweto siku ya Jumapili.
Askofu Mkuu wa Metropolitan, Philip Anyolo, kupitia taarifa yake siku ya Jumatatu, alisema fedha ambazo tayari zilipokelewa zitarejeshwa.
Mnamo Jumapili, Novemba 17, Rais Ruto alichangia KSh 2 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya baba, KSh 600,000 za kwaya hiyo, na kuahidi nyongeza ya KSh 3 milioni kukamilisha nyumba hiyo. Wakati huo huo, Gavana Sakaja alitoa KSh 200,000 kwa kwaya ya parokia na Baraza la Kimisionari la Kipapa (PMC).
Askofu Mkuu wa Metropolitan Philip Anyolo alisema kuwa fedha hizo zitarejeshwa kwa kuwa zilikiuka maagizo ya Kanisa Katoliki na Muswada wa Rufaa wa Kuchangisha Fedha za Umma wa 2024.