SIMBA ipo katika hatua za mwisho za kumrudisha beki wake wa zamani, Shomari Kapombe, baada ya klabu ya AS Cannes ya Ufaransa inayommiliki kwa sasa kuchoshwa na usumbufu wake.
Katika siku za hivi karibuni, Kapombe alidaiwa kuwaniwa na Yanga na Azam FC ili asajiliwe kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na tayari timu zilishafanya naye mazungumzo ya siri.
Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema, Cannes wanaoshikilia haki za Kapombe, wamefikia uamuzi wa kutaka kumuuza beki huyo baada ya kushindwa kuvumilia usumbufu wa mchezaji huyo ambaye hadi sasa bado yupo nchini.
Hanspope alisema, Cannes imewaagiza Simba kulipa gharama walizozitumia katika kumtibu na kuimarisha kiwango cha nyota huyo kwa muda alioishi nchini Ufaransa. Gharama hizo ni Euro 33,000 ambazo ni zaidi ya Sh. 73.1 milioni.
Bosi huyo mwenye nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Simba ambaye kundi la Friends of Simba linataka kumpendekeza kuwania Uenyekiti wa klabu kwenye uchaguzi wa Mei 4, alisema klabu yake imekubali kulipa gharama hizo kwa lengo la kuokoa kipaji cha Kapombe baada ya kubaini mpango wa moja ya klabu za hapa kutaka kumsajili. Kapombe amefungua kesi Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) baada ya Cannes kushindwa kumlipa mshahara wake wa miezi mitatu.
“Simba tupo tayari kumrudisha Kapombe, tumeshazungumza na Cannes wamesema wanataka kurudishiwa gharama zao, pia wapo tayari kushusha zaidi, ndiyo tunasubiri watuambie wanachotaka kutupunguzia ili nasi tujipange kuwalipa, hata mchezaji mwenyewe hana shida katika kurudi hapa,” alisema Hanspope.
Kufuatia taarifa hizo, Mwanaspoti lilimtafuta meneja wa Kapombe ambaye pia ni wakala wake, Denis Kadito anayeishi Uholanzi ambaye alisema anafanya mazungumzo na taasisi kadhaa ili kuokoa kipaji cha mchezaji huyo lakini hakukiri kwamba ni Simba wala hakutaka kufafanua.
“Siwezi kuzungumzia suala la Kapombe kwa sasa, sababu kubwa moja ni kwamba nipo katika mazungumzo na Cannes na taasisi nyingine ili kuokoa kipaji cha mchezaji, naomba mnipe wiki moja nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo,” alisema Kadito.
Aidha Kapombe mwenyewe alipotafutwa alisema:”Sitaki kuzungumzia suala lolote kuhusiana na mpira kwa sasa, kama kuna taarifa zozote umezipata kutoka sehemu nyingine ndiyo hivyo hivyo.”
SOURCE: MWANASPOTI