Mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or ya Real Madrid, Karim Benzema amesaini kujiunga na Al-Ittihad ya Saudi Arabia kwa miaka mitatu kuanzia msimu ujao, chanzo kutoka katika klabu hiyo yenye makao yake mjini Jeddah kiliiambia AFP siku ya Jumanne.
“Benzema amesaini mkataba wa uhamisho wake kwenda Al-Ittihad kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Tangazo hilo linakuja siku chache baada ya Real Madrid kutangaza kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 anaondoka klabuni hapo baada ya misimu 14, siku moja baada ya kocha Carlo Ancelotti kusema “hakuna shaka” mustakabali wa Benzema ulikuwa katika mji mkuu wa Uhispania.
Benzema yuko mbioni kuungana na Cristiano Ronaldo katika ufalme wa Ghuba baada ya Mreno huyo mchezaji bora wa dunia mara tano kuhamia Al Nassr kutoka Manchester United kufuatia Kombe la Dunia mwaka jana.
Mkataba utakuwa halali hadi 2025 lakini pia utajumuisha chaguo kwa msimu zaidi.
Karim atawaaga mashabiki wa Madrid kisha kusafiri hadi Saudia
Benzema alijiunga na Madrid mwaka 2009 akitokea Lyon ya Ligue 1.
Alicheza mechi 647 akiwa na Madrid na anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Real akiwa na mabao 353 — ni Cristiano Ronaldo pekee aliye na zaidi.
Ameinua Ligi ya Mabingwa mara tano, mataji manne ya La Liga na matatu ya Copas del Rey akiwa na Madrid na ndiye anayeshikilia tuzo ya Ballon d’Or ya mchezaji bora wa dunia.
Lakini baada ya msimu mzuri wa 2021-22 alipoiongoza Real kwenye Ligi ya Mabingwa, amekuwa akisumbuliwa na majeraha katika msimu uliomalizika hivi punde na alilazimika kukosa kampeni ya Kombe la Dunia la Ufaransa kutokana na tatizo la paja.