Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amewataka watumishi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kuzingatia maadili na miiko ya taaluma zao ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la NCC jijini Dodoma, Oktoba 23,2024 Mhandisi Kasekenya amesema mahali popote ambapo Baraza la Wafanyakazi likifanya kazi kwa weledi migogoro baina ya Menejimenti na wafanyakazi haitatokea kutokana na kupunguza kero na changamoto baina yao.
“Ni Dhahiri kuwa mahali popote ambapo Mabaraza yanathaminiwa na kufanya kazi ipasavyo, migogoro kati ya Menejimenti na watumishi haiwezi kutokea”’ amesema Kasekenya.
Kasekenya amelitaka Baraza hilo kushirikiana na Menejimenti kuhakikisha wanajadili kwa pamoja masuala ya msingi ya Baraza hilo ikiwemo mipango, Bajeti na masuala mengine ya kiutendaji na kiutawala ili kuweza kufikia malengo na matarajio ya watumishi wa NCC
Amesisitiza umuhimu wa wajumbe na washiriki wote wa Baraza hilo kutumia fursa waliyonayo katika Baraza kuhoji na kutoa mapendekezo chanya yatakayokuwa na msaada kwa NCC na hivyo kuweza kutekeleza majukumu yake katika Sekta ya Ujenzi nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mrisho Mrisho amezungumzia umuhimu wa kila mfanyakazi wa NCC kufanya kazi kwa weledi, uadilifu, kuzingatia miiko na miongozo ya Utumishi wa Umma na hivyo kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa.
“Baraza simamieni maslahi ya watumishi na Menejimenti sikilizeni na kufanyia kazi ushauri wa Baraza kwani ushirikiano baina ya Menejimenti na Baraza utajenga Taasisi imara ya haki na uwajibikaji”, amesisitiza Mrisho
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya NCC, Arch. Dkt. Fatma Mohammed amesema kuwa Baraza hilo litahakikisha maslahi na haki za wafanyakazi zinazingatiwa wakati wote na Menejimenti itatoa ushirikiano wakati wote ili kuleta tija na ufanisi mahali pakazi.