Serikali kupitia Wizara ya Fedha imesema mchango wa Chuo cha Kodi unasaidia kuongeza makusanyo ya Mapato ya Serikali na kuleta uhalisia wa kiutendaji.
“Serikali inajivunia mchango unaotolewa na ITA katika kutoa mafunzo ya Forodha na kodi kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA )na watanzania kwa ujumla kwani yana uhalisia na fursa ya kipekee nchini.”
Hayo yamesemwa na leo Novemba 22,2024 Jijini Dar es salaam na mwakilisha Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Elijah Mwandumbya
katika Mahafali ya 17 ya Chuo cha kodi (ITA) ambapo jumla ya wahitimu 417 wamehitimu katika ngazi mbalimbali.
Amesema wahitimu hao ni wa cheti cha uwakala wa Forodha cha Afrika mashariki (CFFPC), Cheti cha awali cha usimamizi wa Forodha na Kodi(CCTM), Stashahada ya usimamizi wa Forodha na Kodi(DCTM), Shahada ya usimamizi wa Forodha na Kodi (BCTM) pamoja na Stashahada ya uzamili katika Kodi (PGDT).
“Serikali imekuwa ikitambua mchango mkubwa unaofanya na Chuo cha Kodi kwa kutoa mafunzo ili kuwezesha kuwa na watumishi waliobobea na mahili katika ukusanyaji mapato.”Amesema Mwandumbya
Amesema anamatumaini ya kutoa mafunzo katika nyaja za Forodha na Kodi ndio uliopelekea Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanza mchakato wa kufanya Chuo hiki kuwa cha umahiri katika mafunzo haya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwandumbya ameipongeza TRA na Uongozi wa Chuo cha Kodi kwa kufikia viwango hivyo na kueleza kuwa hiyo ina maana kuwa Chuo hicho kina umuhimu na wajibu wa kipekee sio kwa Tanzania bali katika ukanda wa Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla katika kutoa wataalamu mahili katika masuala ya Forodha na kodi.
Pia amekisihi Chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo yenye viwango vya hali ya juu katika kuzingatia maendeleo ya Sayansi na teknolojia kwani ndio nyenzo muhimu katika ufundishaji wa Dunia ya Sasa.
Awali Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Profesa Isaya Jairo amesema Chuo hicho kimetengeneza wataalamu wengi wa Forodha na Kodi katika misingi ya kujenga umahiri wenye kukuza uchumi wa Taifa .
Amesema pia kimekuwa kikitumia fursa za uendeshaji wa teknolojia na sayansi kwa sasa ambayo itawasaidia wahitimu hao kuendana na dunia ya sasa.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Kodi Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika Chuo cha Kodi ikiwemo ujenzi wa hoteli za kisasa .
Dhamira ya Chuo cha Kodi ni kukifanya kuwa cha kimataifa chenye kutoa wahitimu wabobezi katika masuala ya Forodha na Kodi.
Aidha amewapongeza wahitimu kwa hatua waliyofikia na kuwaomba kuwa mabalozi wazuri wa Kodi.