Kenya imeamua kusitisha mpango wa kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti, kama sehemu ya ujumbe wa kimataifa unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, amesema afisa mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya.
Marekani imejibu mara moja: Wizara ya Mambo ya Nje imesema haikuona sababu ya kuchelewesha mpango huu wa kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti.
“Kumekuwa na mabadiliko makubwa kufuatia kuzorota kabisa kwa utulivu wa umma na kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Haiti” Ariel Henry, Korir Sing’oei, katibu kiongozi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, ameliambia shirika la habari la AFP.
“Bila ya utawala wa kisiasa nchini Haiti, hakuna mahali pa msingi ambapo kikosi cha polisi kinaweza kupumzika, kwa hivyo serikali (ya Kenya) itasubiri kutangazwa kwa mamlaka mpya ya kikatiba nchini Haiti kabla ya kuchukua “maamuzi zaidi kuhusu suala hilo,” ameongeza.
Ameongeza kuwa Nairobi, hata hivyo, iko tayari “kutoa uongozi” kwa ujumbe wa kimataifa, ambao uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba.