Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema, Kenya imetoa chanjo kwa karibu watoto milioni 1.9 katika kipindi cha kwanza cha kampeni ya polio.
Kampeni hiyo ya siku tano ilifanyika katika mji mkuu wa Nairobi, kaunti jirani ya za Kiambu na Kajiado, pamoja na kaunti ya Garissa iliyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuwalenga watoto zaidi ya milioni 1.8.
Kampeni hiyo inalenga watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo katika Kaunti ya Garissa.
Kwa mujibu wa WHO, Kenya, pamoja na nchi nyingine katika Pembe ya Afrika, bado ziko hatarini kukabiliwa na mlipuko wa polio kutoka nchi jirani ya Somalia.
WHO imesema kipindi cha pili na cha tatu cha utoaji wa chanjo ya polio kitafanyika mwezi Septemba na Oktoba nchini Kenya.