Mtu huyo aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Kisumu wakati maandamano ya kuipinga serikali yaliyoitishwa na upinzani yakiingia siku ya pili Jumatatu.
Siku ya leo kulishuhudiwa mazingira ya fujo katika jiji la kando ya ziwa huku maafisa wa polisi wa kupambana na fujo wakiendesha vita na umati.
Katika mzozo huo, polisi waliishia kutumia vitoa machozi kuwatawanya baada ya waandamanaji hao kuanza kuwarushia mawe maafisa hao.
Huku hayo yakijiri watu 2 walipigwa baada ya ya polisi kukabiliana na waandamanaji kaunti ya Migori.
Vurugu hizo zilianza Rongo huku waandamanaji waliokuwa na hasira wakikusanyika katika kituo cha Nyarach, ambako Ruto alikaribishwa na kuanza maombi maalum ya kusafisha eneo hilo kabla ya polisi kuwakamata waandamanaji kadhaa.
Katika eneo la Uriri polisi, waliokuwa wamejihami walikuwa katika hali ya tahadhari huku vijana waliokuwa na hasira wakiwa wamebeba mabango na matawi wakiimba dhidi ya mbunge wao Nyamita na rais William Ruto wakiwashutumu kwa gharama ya juu ya maisha.