Utafiti wa shirika la TIFA, umeonesha kuwa asilimia 52 ya wakenya hawana imani na serikali ya rais William Ruto kutokana na kuendelea kupanda kwa gharama ya maisha.
Akizungumza jijini Nairobi wakati wa kutolewa kwa Data ya maoni ya umma kuhusu utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza, Maggie Ireri ambaye ni C.E.O TIFA alifichua kuwa ni asilimia 25 pekee ya Wakenya wanaoamini kuwa nchi inaenda katika mwelekeo unaofaa.
Aidha, utafiti huo umeonesha kuwa kwa kipindi cha miezi 10 iliyopita, raia wa nchi hiyo ambao ni sawa na asilimia 51, wanaamini kuwa kiongozi wao hajatekeleza ahadi alizozitoa.
Raia wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama ya maisha wakitaka serikali kuangazia suala hilo ambalo wanasema limekuwa changamoto kwa raia wa chini.
Upinzani nchini humo ukiongozwa na Raila Odinga, umekuwa ukiwaongoza wafuasi wao kuaandamana kupinga kile wanachosema ni serikali ya rais William Ruto kutoshugulikia suala hilo la mfumuko wa bei za bidhaa.