Wabunge wa Kenya wamepiga kura kuunga mkono muswada unaolenga kupandisha ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) unaotozwa kwa mafuta hadi asilimia 16 kutoka kwa asilimia 8 jambo ambalo linatarajiwa kuongeza gharama ya maisha.
Wabunge Jumatano usiku walipitisha Mswada wa Fedha uliopendekezwa na Rais William Ruto, 2023 na swada huo ulipitishwa baada ya kusomwa kwa tatu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Fedha na Mipango ya Bunge, Kuria Kimani na Sasa itatumwa kwa rais kuidhinisha, ili mapendekezo hayo yawe sheria.
Siku ya Jumatano, wabunge 184 wa muungano wa chama tawala cha Kenya Kwanza walipiga kura kuiidhinisha kifungu hicho ndani ya mswada mpya wa fedha wa mwaka wa 2023, wakati wabunge 88 wakiwemo wa upinzani wakipinga.
Mswada huo ulikuwa na mapendekezo 87 ya marekebisho, baadhi yakiwa yameidhinishwa Jumanne, Bunge la Kitaifa lilipokuwa likizijadili hadi usiku wa manane.
Muhimu kati ya mapendekezo yaliyopitishwa ni ushuru wa asilimia 16 wa ongezeko la thamani kwenye mafuta, kutoka asilimia 8.
Tozo ya nyumba yenye utata, ambayo awali ilipendekezwa kuwa asilimia 3 pia ilipitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho na kuwa asilimia 1.5 ya mishahara ghafi. Ilikuwa imegeuzwa kuwa kodi.
Ushuru wa watayarishi wa kidijitali [content creators]utatozwa kwa asilimia 5 ambapo awali, hii ilipendekezwa kuwa asilimia 15.
Kodi ya zuio ya Kuweka Dau na Bima, ambayo itatozwa kwa asilimia 12.5 na asilimia 16.
Serikali, hata hivyo, inasema kuwa fedha hizi zinahitajika ili kuleta utulivu wa uchumi.
Rais Ruto anasisitiza kuwa utawala wake hautategemea kukopa kufadhili miradi ya serikali na kulipa mishahara.
Serikali rais William Ruto, inatazamia kukusanya takriban shilingi za Kenya 50bn ($356m; £279m) kutokana na kodi ya ziada ambapo imetetea hatua hiyo ikisema inalenga kuboresha maisha ya wakenya katika siku zijazo ikiwa inalenga pia kupunguza madeni yake.
Muswada huo umekashifiwa vikali na wabunge na viongozi wa upinzani wakiongozwa na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga na mashirika mengine yasio ya kiserekali.