Top Stories

Kesi ya Chadema: Viongozi wagoma, Mdee apewa onyo na Hakimu

on

Viongozi saba wa CHADEMA wamesomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, huku wakigoma kujibu chochote kuhusu maelezo hayo.

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo yao na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, ambapo kabla ya kusomewa maelezo yao walikumbushwa mashtaka yao lakini waligoma kujibu kama ni kweli ama lah wamehusika na makosa hayo.

Pia washtakiwa hao waliposomewa maelezo yao ya awali wamedai kuwa hawawezi kujibu kitu kwa kuwa hawajui vifungu vya sheria, pia hawana uwakilishi wa Wakili wao ambaye ni Peter Kibata kwa sababu hayupo mahakamani.

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri amesema ataandika kile ambacho washtakiwa wamekieleza ikiwemo kudai kuwa hawana uwakilishi wa wakili. Pia hakimu huyo amemuonya mshtakiwa Halima Mdee kuacha kumkalipia na asirudie kutoa lugha za namna hiyo.

Kutokana na mvutano wa kisheria na malalamiko ya washtakiwa, wakili wa mbunge Peter Msigwa, Jamhuri Johnson aliamua kujitoa kumtetea Msigwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi November 12,2018.

Washtakiwa waliosomewa maelezo ya awali ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji na mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

BREAKING NEWS: MAHAKAMA YAAMURU MBOWE NA MATIKO WAKAMATWE

Soma na hizi

Tupia Comments