Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Mkoa wa Kilimanjaro imeutaka upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne ili shauri hilo liweze kusikilizwa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Elibariki Philly ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu, Julai 18, 2022 baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili Sabitina Mcharo kuwasilisha ombi la kuitaka mahakama hiyo kutoa tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo kwa madai upelelezi haujakamilika.
“Ikupendeze Mheshimiwa Hakimu, kutokana na upelelezi kutokamilika na pia kibali kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka DPP cha kuipa mahakama hii kibali cha kusikilizwa shaurihili hakijatoka, tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa tena ili tukamilishe upelelezi,” amesema Mcharo.
Mara baadaya maelezo hayo, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Hellen Mahuna pamoja na Fauzia Akonay, ulikuja na malalamiko na kutaka kujua ni kwamini shauri hilo linapigwa kalenda kila inapofika tarehe ya kutajwa.
“Sisi hatuna pingamizi lolote lakini tunamalalamiko, tunataka kujua ni kitu gani kinapelelezwa kwa zaidi ya siku 48, mteja wetu ni mgonjwa sana lakini anajitahidi kufika makahamani, itafika mahali ashindwe kufika na mwisho kesi hii ishindwe kusikilizwa,” alisema Mahuna.
Hakimu Philly ameutaka upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi huo na kukamilisha nyaraka nyingine zinazotakiwa ili shauri hilo liweze kusikilizwa mahakani hapo. Kesi hiyo imeairishwa hadi Julai 29, 2022.