Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa Mamlaka imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso la kufanya maunganisho ya majisafi kwa wananchi wa maeneo ya Kigamboni kwa kutoa vifaa vya maunganisho ya majisafi.
Amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya maunganisho mapya kwa wananchi 45 vilivyokabidhiwa kwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi kwenye ofisi za DAWASA Kigamboni ikiwa ni jitihada za kuchagiza utekelezaji wa ilani ya Chama Tawala kwenye utoaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi.
Ameeleza kuwa hii ni hatua ya awali ambapo wateja 45 waliokwisha kulipia wataungiwa ndani ya siku mbili. Kazi inaendelea ya kuwahasisha wateja wengine 400 ambao wameshapewa makadirio ya gharama ya maunganisho kulipa ili waweze kuunganishiwa na kunufaika na huduma ya majisafi. Sambamba na hiyo amewataka wananchi kuleta maombi ya kupata majisafi ili waweze kufanyiwa upimaji na waweze kunufaika na huduma hii muhimu.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Stanley Mkandawile ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuitikia kilio cha wananchi kuhusu huduma ya maji kwa kutoa vifaa vya kuwaunganisha wateja na majisafi.
Mmoja wa wanufaika wa zoezi la maunganisho mapya Ndugu Yusufu Msabila anaishukuru Mamlaka kwa kumfungia maji nyumbani kwake na sasa anaanza kunufaika na huduma.