Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya kikao cha dharura leo kujadili hali nchini Afghanistan baada ya Wataliban kuuweka mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul chini ya usimamizi wao jana.
Kikao hicho cha hadhara ambacho kitafuatiwa na kingine cha faragha vimependekezwa na Estonia pamoja na Norway.
Ofisi ya Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres imesema Kiongozi huyo anafuatilia yanayotokea Afghanistan na amewahimiza Wataliban na pande zote zinazohusika kuchukua kila tahadhari katika kuyalinda maisha ya Watu na kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji ya kibinadamu.
Ripoti kutoka Afghanistan zinasema kuwa Wataliban wamechukua udhibiti kamili wa Serikali baada ya aliyekuwa Rais wa Nchi hiyo Ashraf Ghani kuikimbia nchi hapo jana.
Marekani imeondoka katika Ubalozi wake kwenye Mji wa Kabul na kuwahamishia Raia wake katika uwanja wa ndege ambao sasa imeuweka chini ya ulinzi wake, Ujerumani pia imewaondoa Raia wake kutoka Afghanistan.