Viongozi wa serikali nchini wametakiwa kuhamasisha wananchi ili waweze kununua na kutumia bidhaa za bima ya afya kwa wote pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu pamoja na matumizi ya bima ikiwemo kwenye mali afya na maeneo mengine yanayohitaji bima.
Wito huo umetolewa na kamishna wa mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dokta Baghayo Sagware wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Njombe ambapo amesema wananchi kwa sasa wanapaswa kupata elimu ya kutosha juu ya bima kabla ya sheria kuanza kutekelezwa kwa kuwa kinachosubiriwa ni kanuni kwa ajili ya kuanza utekelezwaji.
“Wananchi wanatakiwa kuhamasishwa ili waweze kununua na kutumia bidhaa za bima za afya kwa wote,bima hii inaenda kuboresha CHF na kikakacho tokea sasa kila mwananchi wa Tanzania atatakiwa kuwa na bima ya afya na hiyo bima anaweza akanunua CHF,NHIF au anaweza akanunua kwenye kampuni binafsi ambazo zinatoa bima ya afya kwa hiyo kinachosubiriwa ni kanuni na kamishna wa bima atachukua zile kanuni na kusimamia utekelezaji”amesema Dkt Sagware
Kaimu katibu tawala mkoa wa Njombe Edward Mwakipesile amesema viongozi wa mkoa huo wapo tayari kuhamasisha wananchi na kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa bima na kwa kuliona hilo tayari wameanza na kijiji cha Mundindi ambapo serikali ya kijiji imeweza kuwakatia bima wananchi wake wote kwenye kijiji hicho.
“Tumejipanga vizuri na mfano mojawapo ni wananchi wa Mundindi na itakuwa ni chachu kwa sababu swala hilo halitakuwa geni kwetu kwa hiyo tutaendelea na uhamasishaji kuhakikisha wananchi wetu wote tunawashawishi na kuwaelimisha ili waweze kuwa na bima maana afya ni mtaji”amesema Mwakipesile
Nao baadhi ya wananchi wa mkoa wa Njombe akiwemo Ignas Lyimo na Hynes Mbaji wamekiri kuwa bima ya afya ina umuhimu mkubwa kwa kuwa hakuna mtu anayeweza kuwa na fedha wakati wote hivyo kuwa na bima kutasaidia kupata matibabu kwa haraka pindi mwananchi anapopata ugonjwa huku pia bima ya mali ikisaidia kurejesha ahueni yanapowatokea majanga kwenye mali kama maduka kuteketea moto au vyombo vya usafiri kupata ajari.