MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa niaba ya Kamishna Jenerali imeteketeza dawa za kulevya kilogramu 185.35 katika Dampo la Maji ya Chai lililopo wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha.
Pia imeteketeza mirungi kilogramu 154.35 na bangi mbichi kilogramu 31 ambapo jumla ya watuhumiwa watano walikamatwa kwa makosa ya kupatikana na dawa hizo.
Uteketezaji wa dawa hizo ulifanyika wilayani Arumeru mkoani Arusha kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria ambapo Innocent Masangula ambaye ni Mkuu wa Oparesheni kutoka Deca Kanda ya Kaskazini amesema jumla kiasi cha dawa zilizokamatwa na kuteketezwa mbele ya watuhumiwa na kutoa wito kwa wananchi washirikiane na mamlaka katika mapambano hayo.
“Uchomaji wa dawa hizi umezingatoa sheria na Mahakama ya Wilaya ya Arumeru iliridhia vielelezo hivyo viteketezwe kwani uwezekano wa kuleta madhara kwa binadamu ni mkubwa endapo zitaendelea kuhifadhiwa”
Naye Ofisa Sheria wa Mamlaka hiyo, Benson Mwaitenda akizungumza mara baada ya uchomaji vielelezo hivyo amesema sheria ni kali pale mtu akijihusisha na dawa za kulevya kwani anaweza kufungwa miaka 30 au maisha jela na chombo chake kilichotumika kusafirisha au nyumba iliyotumika kama ghala la kuhifadhiwa ikibanikiwa badaa ya uchunguzi kuwa walifanya kwa kujua vinaweza kutaifishwa kuwa mali ya serikali.