Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika barabara ya Wenda-Mgama Km 19 na Mtili-Ifwagi Km 14 katika Wilaya ya Iringa na Mufindi mkoani Iringa.
Barabara hizo zinazojengwa chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Barabara Vijijini kwa Ushirikishaji wa Jamii na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE) zinalenga kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Akiongea katika mahojiano maalum, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mufindi, Mhandisi Richard Sanga amesema kuwa ujenzi wa barabara hizo unalenga kuwezesha wananchi katika shughuli za kilimo na biashara.
“Kukamilika kwa barabara hii ya Mtili – ifwagi kutaiwezesha Wilaya ya Mufindi kufikisha barabara za lami zenye urefu wa Kilomita 87.3 na kuendelea kukuza uchumi wa wananchi”, amesema Mhandisi Sanga.
Naye, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa RISE, Mhandisi Joel Mwandobo amesema ujenzi wa barabara hizo unategemea kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2025 na amemtaka Mkandarasi kampuni ya CHICO kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Barabara Vijijini kwa Ushirikishaji wa Jamii na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE) katika Mikoa ya Iringa, Geita, Tanga na Lindi ili kuendelea kuboresha uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.