Top Stories

Orodha ya vitabu alivyosoma Zitto Kabwe mwaka 2016

on

Upo ule usemi kwamba ukitaka kumficha jambo mtu mweusi basi weka ujumbe kwenye vitabu, hawezi kuuona na eti hilo ni jibu kwamba waafrika hatuna utaratibu wa kusoma vitabu. Hii ni tofauti kwa mwanasiasa maarufu na mbunge wa Kigoma Ujiji, Zitto Zubeir Kabwe ambaye mpaka kufikia sasa ameshasoma vitabu 53.
zitoooooooooKupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto amevitaja vitabu vyote na sababu za yeye kusoma vitabu hivyo pamoja na kile alichojifunza kwenye kila kitabu.

Mwaka 2016 nimesoma vitabu 53. Nimeongeza vitabu nilivyosoma tofauti na mwaka 2015 lakini sikuweza kufikia rekodi yangu ya mwaka 2014 ambapo nilisoma vitabu 56. Hiyo ndio rekodi ya juu zaidi tangu nilipoanza kuorodhesha vitabu nilivyosoma mnamo mwaka 2012. Mwaka 2013 niliorodhesha vitabu vichache zaidi nilivyosoma.

Mafanikio makubwa ya mwaka huu ni kuongeza vitabu vya Riwaya (fiction), ingawa mtaona mwandishi mmoja, Jeffrey Archer amejitokeza sana kuliko wengine. Hiyo ni kutokana na kusoma kazi yake moja nzuri na yenye mafunzo mengi sana kwa wanasiasa iitwayo First Among Equals. Kazi hiyo ilinifungua macho na kuanza kusoma Clifton Chronicles (vitabu 7) na kufuatia mapendekezo ya wanaonifuata kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram niliweza kupata vitabu vingine vya mwandishi huyu. Kwangu mimi ndugu Jeffrey Archer ni Mwandishi wa Riwaya Bora wa Mwaka 2016.

Licha ya kutaka kuanza na Gavana Ben Bernanke, nilijikuta naanza na vitabu kuhusu Russia na Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin. Msukumo huo ulitokana na namna nilivyomsoma Mtawala mpya wa Tanzania, Rais John Magufuli kulinganisha na mtangulizi wake, Kiongozi wa zamani wa nchi yetu, Rais Jakaya Kikwete.

Kitabu nilichoanza nacho mwaka 2016 ni “The Strongman: Vladimir Putin and the Struggle for Russia” kilichoandikwa na Angus Roxburgh. Baada ya kusoma kitabu hiki nilijikuta ninanunua vitabu vingi kuhusu Urusi, Putin, Udikteta, Demokrasia na Maendeleo ili kuweza kuelewa mwelekeo wa Siasa za Tanzania za sasa.

Vitabu hivyo vimenisaidia sana kujua namna ya kutafsiri watawala wapya kiasi cha kuunda neno “Dikteta Mamboleo” (neo-dictatorship) na kuipa tafsiri yake mnamo tarehe 29 Septemba 2016; kwamba Dikteta Mamboleo ni mtawala ambaye ana uzalendo usiotiliwa shaka na anahangaika kuleta maendeleo ya nchi yake lakini hataki kuhojiwa kwa namna yeyote ile.

Mwaka 2016 pia ulinifunua kuhusu uwezo mkubwa na umahiri wa wachapishaji wa Vitabu wa ndani. Nilipata fursa adhimu ya kuzungumza na Mzee Walter Bgoya wa Mkuki na Nyota Publishers. Vitabu kadhaa nilivyosoma katika orodha ya mwaka huu vimechapishwa na Mkuki na Nyota. Nimejifunza changamoto zao na pia mafanikio ya wachapishaji wa ndani.

Nilijifunza mengi mapya ya historia ya nchi yetu na Afrika nzima. Juzuu za masimulizi ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika nilizipata kutoka Mkuki na Nyota na humo nilipata mambo mapya mengi sana. Kisa kimoja kinachonichekesha kila nikumbukapo ni hadithi ya Rais Seretse Khama, baba wa Taifa wa Botswana, alivyobeba machungwa kwenye ndege kumletea zawadi Mwalimu Nyerere, akimtania kuwa sera zake za Ujamaa zilileta njaa nchini. Lakini zaidi nikijifunza Uzalendo, Umajumui wa Afrika na namna wazee wetu walivyojitoa kwa ajili ya bara hili.

Mwaka huu tumeunda “Klabu ya Usomaji wa Vitabu ya Wabunge”, napenda kuwashukuru wabunge wenzangu wote walio kwenye klabu hii, mchango wao kwangu ni mkubwa sana. Kipekee nimshukuru Kiongozi wetu wa klabu hii, mama yangu, Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, hamasa yake kwetu wabunge vijana ni mchango wake muhimu sana kwa Taifa.

Niwashukuru pia kaka zangu January Makamba, Daktari Hamisi Kigwangalla na ndugu Ezekiel Kamwaga kwa vitabu walivyopendekeza, kunipa au kuniazima katika mwaka huu. Ahsanteni sana ndugu zangu.

Mwaka huu ninawawekea mapema vitabu nilivyosoma tofauti na miaka iliyopita kwa sababu kwa uwezo wake Manani sitaweza kusoma vitabu vingine baada ya leo kwani nitakuwa na majukumu ya Malezi.

Karibuni kwenye orodha ya vitabu vyangu mwaka 2016.

zitto-1 zitto-2 zitto-3 zitto-4

Natumaini Mola akinipa Uhai mwakani nitasoma vitabu vingi zaidi na kuvunja rekodi yangu ya vitabu 56 ya mwaka 2014. Nichukue nafasi hii kuwatakia ndugu zangu, watanzania wenzangu kheri za sikukuu hizi za mwisho wa mwaka.

VIDEO: Ukimuuliza ZITTO KABWE leo kuhusu mapendekezo yake kwenye Elimu ya Tanzania atakujibu hivi. Bonyeza play kwenye video hapa chini

Soma na hizi

Tupia Comments