Kiongozi wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais wa Gabon Ali Bongo aliapishwa kama rais wa mpito na majaji wa mahakama ya kikatiba siku ya Jumatatu katika hafla ya televisheni iliyobuniwa kuimarisha utawala wa serikali.
Katika mapinduzi ya nane ya Afrika Magharibi na Kati katika kipindi cha miaka mitatu, maofisa wa kijeshi wakiongozwa na Jenerali Brice Oligui Nguema walichukua mamlaka Agosti 30, dakika chache baada ya tangazo kwamba Bongo amepata muhula wa tatu katika uchaguzi – matokeo waliyoyabatilisha na kusema hayakuwa ya kuaminika. .
Nguema alipokelewa kwa shangwe na hadhara ya maofisa wa kijeshi na viongozi alipowasili kwa ajili ya sherehe hizo, na tena mara tu baada ya kuapishwa. Televisheni ya Taifa ilionyesha picha za umati wa watu wenye furaha na vifaru vikifyatulia risasi baharini kuashiria tukio hilo.
Mapinduzi hayo, ambayo yalimaliza miaka 56 ya familia ya Bongo madarakani katika nchi hiyo inayozalisha mafuta, yalivuta umati wa watu waliokuwa wakishangilia katika mitaa ya mji mkuu Libreville lakini kulaaniwa kutoka nje ya nchi.