Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, CDC, kinasema mlipuko wa mpox barani Afrika bado haujadhibitiwa na kuongeza kuwa maambukizo yameendelea kuripotiwa kwenye mataifa kadhaa.
Shirika la Afya duniani, WHO, lilitangaza mlipuko huu kuwa hali ya dharura ya afya ya umma, siku chache kupita tangu virusi hivi vipya kutambuliwa.
Nchi za Afrika zinaendelea na juhudu za kukabiliana na mlipuko mwingine unaotokea baada ya janga la COVID-19 ambalo lilionesha udhaifu wa mifumo ya kiafya kwa bara hilo, mifumo ambayo haikuwa tayari kumudu janga kama hili.
Mkurugunzi wa CDC, Jean Kaseya amesema kasi ya maambukizi mapya imefikia asilimia 177, vifo vikiwa asilimia 38.5 ikilinganishwa na mwaka jana, mataifa 15 ya Afrika yakiwa yameripoti maambukizo.
Ukosefu wa uwezo, chanjo na nyezo za kupima watu ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha bara hili kujua kiwango cha maambukizo kwenye nchi nyingine.