Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba amezindua kiwanda cha kutengeneza Transformer cha kampuni ya Elsewedy Electric kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Kigamboni wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa, Balozi wa Misri nchini Tanzania Mheshimiwa Mohamed Jaber Abu El Wafaa, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Maharage Chande na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Said.
Akitoa taarifa kuhusu kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Elsewedy Electric kwa Kanda ya Afrika Mashariki, Mhandisi Ibrahim Qamar alisema kuwa ujenzi huo ni wa awamu ya pili ambao utawezesha kiwanda kuwa na uwezo wa kuzalisha transformer 2,500 kwa mwaka kwa ajili ya soko la ndani pamoja na kuuza nchi za nje ikiwa pamoja na Kenya, Madagascar, Rwanda, DRC, Zimbabwe na Afrika ya kusini. Pia watatarajia kuajira kwa Watanzania zaidi ya 1,500 na kuwajengea uwezo vijana wanaomaliza vyuo pamoja na kujenga Chuo cha Ufundi.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kiwanda hicho ilizinduliwa Desemba 2021 na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa kiwanda hicho mbali na Transformer, kinazalisha pia vifaa vya umeme vikiwemo Nyaya na mita ambazo wateja wake wakubwa ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Aliongeza kuwa tayari REA kupitia Wakandarasi wake wanaosambaza umeme vijijini wameanza kutumia vifaa vinavyotengenezwa na kiwanda hicho.
Waziri Makamba aliipongeza Serikali ya Misri kupitia Balozi wake pamoja na uongozi wa Kampuni ya Elsewedy Electric kwa ujenzi wa Awamu ya Pili.
“Nawahakikishia soko la Transformer hizo kwani kazi ya usambazaji umeme mijini, vijijini pamoja na vitongoji inaendelea. Vile vile muongeze uzalishaji wa Transformer kwani katika kipindi cha miaka 5 kuanzia sasa zitahitajika Transformer 40,000 kwa ajili ya kupeleka umeme vitongojini na Transformer nyingine 50,000 kwa ajili ya Miradi ya TANESCO” alisema Waziri Makamba.
Alisisitiza kuwa Serikali inategemea kuwa bei ya Transformer hizo zitakuwa chini ikilinganishwa na bei ya ya Transformer zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Aidha, aliitaka Kampuni hiyo kuzalisha Transformer zenye uwezo mkubwa (Power Transformers) ambazo kwasasa zinaagizwa nje kwa gharama kubwa na huchukua muda mrefu kuwasili nchini.
Waziri Makamba, alimuhakikishia Balozi wa Misri na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni hiyo pamoja na Sekta binafsi kwa ujumla kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.