Leo January 9, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Lowassa amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri na ametaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji, ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa.
Namnukuu Lowassa >>>“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo,”
“Moja na kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira,”- Lowassa
“Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mengine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, kwa kweli nakushukuru Rais, you made my day” – Lowassa.
Rais Magufuli amempongeza Edward Ngoyai Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema Lowassa ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake ametoa mchango wake katika nchi.
President Magufuli amesema kuwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.
“Ameniomba mara nyingi nikutane nae na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, kama alivyosema tumefanya mambo mazuri mengi.”– President Magufuli
“Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Trilioni 7, juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji, elimu bure, huduma za hospitali na mengine” -President Magufuli.